Somo la Kwanza
Mdo 13:14, 43-52
Wimbo wa Katikati
Zab 100: 1-3, 5
Somo la Pili
Ufu 7:9,14b-17
Shangilio
Yn 10:14
Somo la Injili
Yn 10:27-30
Yesu alisema; Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu. Mimi na Baba tu umoja.
Katikati ya msitu wa makelele ya ulimwengu, Neno la Mungu bado linasikika masikioni mwetu. Uthibitisho wake ni Miito mitakatifu katika Kanisa, Ndoa, Utawa, Upadre na pia wito wa Kazi katika jamii. Sote tunapofuata wito wetu kwa uaminifu tunakuwa kondoo wanaosikia na kusikiliza sauti ya Mchungaji, Kristo Bwana wetu. Tuombee Miito mitakatifu katika kanisa letu.
Somo la I: Paulo na Barnabas wanaitikia wito wa Kristo mfufuka kwa kuihubiri Injili. Watu wa mataifa na baadhi ya Wayahudi wanaongoka na kufurahia Injili/Neno la Mungu. Kazi yetu kama wabatizwa tumaitwa kuihubiri Injili. Kuleta furaha na wongofu kwa watu. Zaidi kwa waliowekwa wakfu, mapadre na watawa, ndio kazi yao ya kwanza kuhubiri Injili na kuokoa roho za watu. Lakini hawa watu wa Mungu ni kwa namna gani wanafanyika? Wimbo wa Mwanzo umetuambia, kwa Neno la Bwana Tunafanywa hivi tulivyo: Upadre, utawa, Ndoa, kazi, n.k
Makelele yapo katika ulimwengu na yanaizonga kazi ya Mungu. Paulo anataja machache. Wivu: Wayahudi wanakasirika na kuwa na wivu kwa makutano yaliyokusanyika kulisikia Neno la Mungu. Fitina: Wayahudi walipozidiwa na Neno la Bwana kuenea nchi ile yote, waliwafitinisha wanawake kuharibu kazi ya Paulo na Barnaba. Mambo hayo yapo hata sasa. Wapo wanaokwamisha miito mitakatifu; kuwakatisha tamaa, kuwasingizia, kuzushia fitina, kuwasema vibaya hata kwa wasioyatenda. Wapo pia wanaokwamisha ndoa za wengine, wanaovuruga mipango ya ndoa takatifu, wanaokuwa wagumu kufunga ndoa n.k. Hii ni kukwamisha kondoo wasiisikie na kufuata sauti ya Mchungaji.
Somo la II: Somo la pili linatupa matumaini ya kipasaka. Kwamba kwa kuisikia sauti ya Mungu, kuwa kulisikia Neno la Mungu, vikwazo vipo, majaribu yapo, kukataliwa kupo, kukwamishwa kupo. Mashahidi anaowaona Yohane katika ufunuo wake, ni wale walioosha mavazi yao katika damu ya mwanakondoo. Kama Kristo alivyoshinda kukataliwa, kuteswa, kuuwawa, kadhalika nasi kondoo wake kwa kuisikia sauti yake na kumfuata lazima kushinda makelele na makwazo ya ulimwenguni. Sharti ni kujikabidhi kwake anayetuongoza kwenye chemchemi ya maji yenye uhai na Mungu atafuta machozi ya mateso na taabu zetu.
Injili: Yesu ndiye anayeita. Ndiye Mchungaji anayetuita na kutuchunga sisi Kondoo wake. Sharti kwetu sisi ni kuitikia, kuisikia na kusikiliza sauti yake, na kumfuata. Tuzo anayotupa ni uzima wa milele. Ndiye anayekamilisha kile alichokianzisha ndani yetu kwa kupitia kanisa anapowainua watu wake kuwachunga kondoo wake. Hivyo tunaposikiliza wachungaji wetu, tunamsikiliza yeye aliyewaita na kuwachagua kati ya watu kuwaongoza watu.
Kanisa chini ya Mchungaji Mwema limekuwa likipata zawadi ya miito mitakatifu. Wito wa kwanza ni wa kuwa mwanadamu. Mungu ametaka tuwe tulivyo sio kwa bahati mbaya bali kwa makusudi yake. Hakuna aliyechagua kuzaliwa. Mungu kwa upendo wake katuumba, tena kwa sura na mfano wake, na akatupa uhai – ndio maana tunaalikwa kuudhamini uhai tangu tumboni. Hatuna ruhusa ya kuharibu uhai kwa namna yoyote ile, kwani ndio msingi wa miito mitakakatifu na miito yote. Ndio maana kutoa mimba ni kinyme na mpango wa Mungu, kutumia kinga kuzuia mimba ni kinyme na mpango wa Mungu. Wanaoshabikia hayo – ndio Kondoo wasioisikia sauti ya Mchungaji.
Miito mitakatifu huzaliwa ndani katika ubinadamu wetu, katika familia zetu, Ndio maana hatuwezi kuzungumzia wito wa upadre na utawa bila wito wa ndoa takatifu. Mapadre na watawa wanazaliwa katika familia. Mapadre na watawa wanatolea maisha yao kwa ajili ya kumtumikia Mungu na kuwahudumia watu, kwa ajili ya kondoo wa Mungu, kuwaelekeza kondoo kuisikia sauti ya Mchungaji Mwema. Ndio maana leo ni siku ya kuombea miito hiyo mitakatifu na zaidi kuombea familia zetu, ndoa zetu ili kusudi miito mitakatifu iendelee kuchipua katika familia zetu.
Tunamshukuru Mungu kwa ajili ya wale wanaoombea miito mitakatifu na kuwa Support kwa namna mbalimbali katika kanisa, ndio namna ya kuwa kondoo wema wanaosikia sauti ya Mchungaji.
Yesu ndiye Mchungaji Mwema, na kwa wema wake anawainua wachungaji, mapadre kati yetu kwa ajili ya kuwachunga kondoo zake. Ili sote tuisikie sauti yake katikati ya makelele ya sauti nyingi, tuupate uzima wa milele. Licha ya changamoto za ulimwengu, ahadi yake Yesu ni kwamba tunapowakabidhi wachungaji wetu mikononi mwake, hakuna anayeweza kumuibia. Tuwaombee mapadre, watawa, na miito mitakatifu katika kanisa. Amina.