Somo la Kwanza: Mdo 14:21b-27
Wimbo wa Katikati: Zab 145:8-13
Somo la Pili: Ufu 21:1-5a
Shangilio: Yn 13:34
Somo la Injili
Yn 13:31-33a, 34-35
Yuda alipokwisha kutoka, Yesu alisema, Sasa ametukuzwa Mwana wa Adamu, naye Mungu ametukuzwa ndani yake.
Mungu naye atamtukuza ndani ya nafsi yake; naye atamtukuza mara. Enyi watoto wadogo, bado kitambo kidogo nipo pamoja nanyi; Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.
Utangulizi: Katika Dominika ya leo tunakumbushwa kuhusu upendo. Kupendana sisi kwa sisi. Na kwa upendo wetu tunatambulika sisi ni akina nani! “Naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake”
Tafakari: Kwa kupenda tunatambulika sisi ni akina nani. Mungu amejulikana kwetu kwa sababu ya upendo wake kwetu, na kwa kumpenda yeye tunajua sisi ni kina nani kwake. na tunapopendana tunajulikana kwa ulimwengu kuwa sisi ni wakristo, na ndio njia ya kumpenda Mungu.
Somo la I: Katika somo la kwanza tunaona nguvu ya Mungu kwa Paulo na Barnaba huko wanaporudi Litria, Ikonio na Antiokia. Kule walikopanda mbegu ya Ukristo. Ndiko Yesu aliposia mbegu ya upendo kwa watu wa mataifa na kuitwa wakristo. Wanawaimarisha na kuchagua wazee/viongozi wa kuliongoza kanisa.
Leo hii Mbegu hii ya upendo wa Kristo wa Imani yetu, je unazungumza kwa watu? unazungumza kwa ulimwengu?. Unapojitambulisha Mkristo/sisi ni wakristo! Je watu wataona Msema kweli?, Anayejali wengine? anayeheshimu wengine? anayependa wengine? anayependa haki? anayejitahidi kuishi Imani yake? Ni nini kitakacho kutambulisha wewe ni mfuasi/mwanafunzi wa Yesu?.
Somo la II: Jamii ya wakristo wakwanza sio kwamba pia wao walikuwa watakatifu. Ndio maana Paulo anawaimarisha. Na katika somo pili kutoka kitabu cha Ufunuo, Yohane anatuambia Mji mpya Yesusalemu, mji ule mtakatifu utashuka kutoka mbinguni kwa Mungu. Mji huo hautatoka duniani kwa sababu ya udhaifu na mapungufu yetu ya kibinadamu. Lakini bado Ukristo wetu (kanisa) duniani ni kitalu cha Yesu kusia mbegu ya Ukweli na Upendo.
Injili: Katika karamu ya mwisho kabla ya kuteswa kwake, Yesu aliwaachia wanafunzi wake wosia wa Kupendana. Hii ndio amri mpya, hii ndio amri yetu wakristo kupendana sisi kwa sisi. Upendo ndio alama ya utambulisho wa Ukristo wetu. Upendo si neno geni katika masikio yetu. Neno hilo upendo linatumika maara nyingi katika maisha yetu. Mfano, upendo kwa nchi yangu, napenda kazi yangu, napenda wazazi wangu, napenda familia yangu, nawapenda marafiki zangu, nampenda mke wangu/mume wangu, nampenda mchumba wangu, n.k. Yote haya yanazungumzia upendo lakini wataalamu wanatuambia huu unaweza kuwekwa katika makundi mawili eros na philia. Ni upendo unaoanza chini kwetu ndo unapanda juu. Kwamba unampenda mtu au kitu kwa sababu fulani ama kwa kuwa unafaidi kitu fulani. Huu haututambulishi sisi kuwa wafuasi wa Kristo. Ndo maana Yesu aliuliza, “mkiwapenda wanaowapenda mwapata faida gani (Mt 5:46).” Kama hata ukijitoa vipi kwa mali kama motif ya majitoleo si upendo, basi haifaidii kitu (1Kor 13:3).
Upendo anaozungumzia Yesu unatoka juu. Ni upendo wa kweli, wa kujitoa kwa ajili ya wengine bila kutarajia chochote. Selfless love. Ndio maana mfano anaoutumia ni wa “Kama vile nilivyowapenda ninyi” nanyi “Mpendane”. Tofauti na ule upendo mwingine upendo huu unatoka juu, unaanzia kwa Yesu mwenyewe. Ndio upendo unaotutambulisha kuwa sisi ni wafuasi wa Kristo. Na tukifanya hivyo tutakuwa mashahidi wa Injili ulimwenduni.
Kupenda kama Kristo alivyotupenda haiwezekani. Hivyo inahitaji kwanza uwepo wake katika maisha yetu, katika roho zetu, katika fikra zetu, katika mtazamo wetu ili tuweze kupenda kama yeye alivyotupenda.
Hivyo tunahitaji kupendana sisi kwa sisi ili kusudi ulimwengu uweze kumtambua Kristo. Upendo huo wa kweli ni upi? Kwanza tumeambiwa ni ule unaofanana na wa Kristo. Pili, Paulo anatuambia upendo una sifa zifuatazo; Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauhusudu, hautakabari, haujivuni, haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, hauoni uchungu, hauhesabu mabaya, haufurahii udhalimu, huvumilia yote, haupungui neno wakati wowote (1 kor 13:4-8).
Tumwombe Kristo atujalie kupendana. Licha ya ubinadamu wetu, bado Kristo anasia mbegu ya upendo na ukweli ndani mwetu ili ulimwengu uzidi kumtambua yeye.