Kwa Matumaini Tunaokolewa

2025-05-25
Dominika ya 6 ya Pasaka
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
šŸ“– Masomo ya Dominika

Somo la Kwanza: Mdo 15:1-2, 22-29
Wimbo wa Katikati: Zab 67:1-5, 7
Somo la Pili: Ufu 21:10-14, 22-23
Shangilio: Yn 14:23

Somo la Injili
Yn 14:23-29
Yesu aliwaambia wafuasi wake, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka. Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu. Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga. Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba, kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi. Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini. Neno la Bwana.

šŸŖ” Tafakari ya Neno

Utangulizi:
Tumezoea kupanga mambo ya siku za mbeleni kwa matumaini Imani kubwa. Mipango Mipango yetu mara nyingi utasikia kesho, kesho kutwa, wiki lijalo, mwezi/miezi ijayo, mwaka/miaka ijayo. Matumaini haya ni makubwa ya kuishi na kutekeleza majukumu yetu ya sasa na wakati ujao. Katika Dominika ya leo Yesu anatufunulia kwamba tunaweza kuishi matumaini hayo katika mambo makuu matatu; katika Neno lake, katika Amani na katika Roho Mtakatifu.

Tafakari:
Somo la I: Katika somo la kwanza tunasoma sehemu ya mtaguso wa kwanza wa Yerusalemu kuhusu tatizo la kuongezeka kwa wapagani/watu wa mataifa katika jamii ya Wakristo. Wakristo hao wanapoongezeka, wanaanza kubaguliwa. Kwamba wasipotahiriwa hawawezi kuokoka. Ubaguzi umekuwa janga la ulimwengu wa sasa. Ubaguzi umekuwa hata wa wazi katika mazingira yetu.
Pengine tumekuwa tunabagua watu kwa tamaduni zetu, uwezo wetu, dini zetu, kabila zetu, kazi zetu, madaraka yetu, n.k. Hapa tunaharibu mambo ya msingi anayotufundisha Yesu. Neno Lake ni kwa ajili ya watu wote. Amani ni zawadi aliyotuachia ili tuweze kuishi na kila mtu na kuhusiana na kila mtu kwa upendo. Roho Mtakatifu anayetuunganisha wote. Mitume na wazee wanawaasa watu wa Antiokia kuwa vitu vinavyoleta ubaguzi ni dhambi, matambiko na kuabudu miungu mingine.

Somo la II: Ishara ya mji wa Yerusalemu ya mbinguni ni mji wa kudumu. Wenye umungu ndani yake, unaong’aa kwa utukufu wa mwanakondoo (divine glory & nature). Ishara hii ya mji wenye misingi uliondikwa majina kumi na mbili ya mitume ni ishara ya kanisa lililojegwa juu ya mitume na lina umungu ndani yake. Ndilo kanisa linalohubiri Neno la Mungu, amani na kutupa mapaji ya Roho Mtakatifu. Hivyo kanisa ni kitalu cha matumaini.

Injili: Yesu anawaimarisha wanafunzi wake na kuwaahidia Roho Mtakatifu. Ahadi hii kuu ya Yesu, ya upendo kwa neno lake, ya kutuombea amani na ya Msaidizi, ndio inayotupa matumaini makubwa si tu ya kuishi sasa bali kupata wokovu wa milele. Yeye mwenyewe ndiye tumaini la kwanza katika Neno lake. Licha ya kwamba anawapa wosia wanafunzi wake, lakini Neno lake Mwenyewe kwa wanafunzi wake linawaimarisha. Na neno lake ni kumpenda yeye tu, na baba atampenda. Upendo huo unajidhihirisha kwa kutii Neno Lake. Tunalishikaje neno lake?, Kwa kusoma Biblia, kushika amri zake, wajibu wetu kwa kanisa, majitoleo yetu, kusali n.k.
Tukishika Neno lake, anatupa amani. Amani hii sio ya kiulimwengu. Ni amani ya ndani. Licha ya fujo za ulimwengu na za maisha, amani ya Yesu ni ya pekee. Inatuliza mioyo yetu. Tumezoea watu kusema nina amani baada ya kupata kitu fulani, kufaulu jambo fulani, kushinda kitu fulani, n.k. Amani ya Yesu hutupa furaha na utulivu iwe tumepata au hatujapata, iwe tumefaulu ama hatujafaulu, iwe tunateseka au tunafurahi, iwe tumeshindwa au tumeshinda, iwe tu wagonjwa au wazima. Amani yake hutawala nyakati zote. Ndio hutupatia matumaini wakati wote. Ndiyo inaitwa ā€œthe tranquillity of orderā€.

Tumaini kubwa zaidi tunaloahidiwa ni la ā€˜msaidizi’. Huyo Roho Mtakatifu ambaye Baba atampeleka ndiye atakayewafundisha yote na kuwakumbusha yote. Ndugu zangu ukimtoa Roho Mtakatifu katika kanisa, kanisa linasambaratika ndani ya sekunde. Ukimtoa Roho Mtakatifu katika maisha yetu, hatutafanikiwa kwa chochote (Rum 8:26-27). Hilo ndilo tumaini na imani kubwa anayotupa Yesu katika wosia wake kwa wanafunzia wake, hasa kutuahidia huyo ā€˜Msaidizi’. Huu ndio uhakika wa maisha yetu yajayo na hasa ya uzima wa milele.
Kupitia Neno lake Yesu, amani yake, na Roho Mtakatifu anayempeleka kwetu, tunapata matumaini makubwa katika kupambana na changamoto, magumu na shida yoyote katika maisha yetu. Ndio kusema Yesu anatimiza ahadi yake ya kuwa nasi katika maisha yetu hadi mwisho wa nyakati. Kanisa limesimama imara na linadumu tokea mtaguso wa Yerusalemu kwa sababu ya ahadi hiyo. Nasi tukimtegemea Yesu katika Neno lake, amani yake na Roho Mtakatifu tutashinda katika changamoto zetu.